Mbaroni kwa kuzuia kidato cha 4 kufanya mtihani

21:33

POLISI mkoani Dodoma inawashikilia walimu watatu wa shule za sekondari kwa tuhuma ya kuwazuia wanafunzi wa kidato cha nne, kufanya Mtihani wa Taifa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Lazaro Mambosasa alisema kwamba walimu hao wa shule za sekondari za Zoissa na Mnyakongo wilayani Kongwa, walikamatwa Novemba Mosi mwaka huu.

Kamanda Mambosasa alisema kwamba, wakati wa mtihani wa somo la Kiingereza, walimu hao walimzuia mwanafunzi Amina Said wa shule ya sekondari Zoissa kwa madai ya kuwa ni mjamzito na kumpeleka kituo cha afya, kupimwa muda wa mtihani, lakini majibu yalionesha hakuwa na ujauzito.

Aidha, mwanafunzi Bahati Ntigonza wa shule ya sekondari Mnyakongo, alizuiliwa kuingia katika chumba cha mtihani kwa kuwa hakuvaa sare ya viatu, hivyo alirudishwa nyumbani kuvaa viatu huku wenzake wakiendelea na mtihani.

Kamanda Mambosasa aliwataja watuhumiwa waliokamatwa kuwa ni Lukonge Mwezo ambaye ni Mkuu wa Shule ya Sekondari Mnyakongo, Omari Athumani Mkuu wa Shule ya Sekondari Zoissa na Daud Suleimani John aliyekuwa mwalimu wa zamu katika shule ya sekondari Mnyakongo.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »